Breaking News
recent

Askofu amfananisha Rais Magufuli na Yesu Kristo......Asema Hata Yesu Alisisitiza Juu ya Ulipaji wa Kodi na Ushuru



Askofu mstaafu wa kanisa la Pentekoste (FPCT)  Singida mjini Dk. Paul Samweli, amesema suala la serikali ya Dk.  John Magufuli kusisitiza ulipaji wa kodi na ushuru ni utekelezaji wa maagizo ya Yesu Kristo,  hivyo waumini na Watanzania kwa ujumla, wanatakiwa kutii na kuzingatia wajibu wao huo.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, amesema kwa mujibu wa kitabu kitakatifu cha Mungu  cha biblia Warumi 13  (msitari 1-14), inaonesha wazi Yesu kristo alipigia debe Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).

Askofu Paul alisema katika Warumi 13  kimeainisha kuwa watoza kodi na ushuru, ni wahudumu wa Mungu kuwa wapeni haki zao, mtu wa kodi, kodi, mtu wa ushuru, ushuru.

Dk. Paul amesema hayo juzi wakati akihubiri kwenye ibada ya kawaida ambayo pia ilihudhuriwa na kamanda wa jeshi la polisi  mkoa mkoani  hapa ACP Debora Daudi Magiligimba.

Akisisitiza, alisema kwa vile ulipaji   kodi umepewa baraka zote na Mwenyezi Mungu, waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini, wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutii agizo la Mungu la kulipa kodi uliowekwa kisheria bila shurti.

“Serikali ya Rais Magufuli katika hili la uhimizaji wa ulipaji kodi na ushuru, inafanya vizuri kazi iliyopo mbele yetu waumini wa dini na Watanzania kwa ujumla, ni kulipa kodi na ushuru kwa wakati, ili nchi yetu iweze kusonga mbele kimaendeleo. Haya mambo ya  kukwepa kulipa kodi au ushuru, yakomeshwe,” alisema.

Kuhusu watoza kodi na ushuru Dk.Paul, alisema kuwa katika Biblia (Luka Mtakatifu 3 -12-17)  inasema  watoza kodi/ushuru waliagizwa wasitoze kubwa ambayo itakuwa kinyume na sheria inavyoagiza.

Akifafanua, alisema wafanyakazi wa TRA, katika utekelezaji wa majukumu yao, wanatakiwa kutoza kodi na ushuru kwa mujibu na sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na si vinginevyo.

“Wakitoza kodi au ushuru mkubwa ambao upo  kinyume na sheria, watakuwa wanamudhulumu mlipaji, kitendo hicho sio tu binadamu mwenye maadili mema hakipendi, lakini pia, nacho hakitampendeza Mwenyezi Mungu,” alisema.

Kwaupande wa jeshi la polisi, Dk. Paul amesema kwamba katika kitabu cha Warumi 3 mstari wa 14, kimewataka askari polisi katika kutekeleza majukumu yao, wasidhulumu mtu wala wasiwababikizie watu kesi za uongo. Pia watosheke na mshahara wanaolipwa.

“Kamanda maneno yaliyotamkwa  na mtumishi wa Mungu Yohana, yanamtaka  kila askari polisi, aridhike na mshahara wake. Ina maana asiwe na tamaa ya kuomba rushwa na vile vile asibabikie  mwananchi kesi, bali atatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba wake wa kazi,” alisema.

Dk. Paul alitumia  fursa hiyo kulipongeza jeshi la polisi mkoa wa Singida kwa juhudi zake za kudhibiti vitendo vya kihalifu ambavyo vinaweza kuhatalisha amani na utulivu ulipo.

“Nikupongeze kipekee kamanda Magiligimba kwa kuazisha utamaduni mpya wa kuongea na waumini wa madhehebu ya dini kwenye nyumba zao ibada. Pia kwa uamuzi wako wa kudhibiti uhalifu kabla haujatokea. Kwa kifupi unataka dalili za kutokea uhalifu, zishughulikiwe mapema kabla hazijaleta madhara. Sisi kanisa tunakuunga mkono katika hili. Mungu akutangulie,” alisema Dk.Paul.

No comments:

Powered by Blogger.